BASATA YAMTOZA HARMONIZE FAINI YA SH5 MILIONI
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemtoza msanii Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ faini ya Sh5 milioni kwa tuhuma za kusambaza video ya wimbo wake “Kudos”, ambayo limeeleza kuwa inakiuka maadili ya Mtanzania.
Kwa mujibu wa BASATA, Harmonize hakuwasilisha utetezi wala maelezo mbadala kuhusu tuhuma hizo hadi wakati wa kutolewa kwa uamuzi.
Mbali na faini hiyo, BASATA imemuamuru Harmonize kuiondoa video hiyo kwenye mitandao yake ya kijamii na kusitisha shughuli zote za sanaa hadi atakapotekeleza maamuzi hayo.
Muongozaji wa video hiyo, Kennedy David Sanga ‘Dir. Kenny’, naye ametozwa faini ya Sh5 milioni. Pia ameagizwa kuiondoa video hiyo kwenye mitandao yake na kusitisha shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza uamuzi huo.
Wakati huo huo, msanii Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ ametozwa faini ya Sh3 milioni baada ya kukiri kosa la kuvaa mavazi ambayo BASATA imesema hayakuwa na staha wakati akitumbuiza katika fainali ya Miss Universe Tanzania 2026.
BASATA imesema Nandy tayari ameiondoa video hiyo kwenye mitandao yake na kulipa faini, hivyo ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake za sanaa chini ya uangalizi.
Katika taarifa hiyo, BASATA imewataka wasanii na wadau wa sanaa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maadili ya Mtanzania wanapotekeleza shughuli zao.