BASATA Yamtoza Dudu Baya Faini ya Sh3 Milioni
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemtaka msanii Godfrey Tumaini, maarufu kama Dudu Baya, kulipa faini ya shilingi milioni tatu ndani ya siku 14 kufuatia ukiukaji wa mwongozo wa maadili ya sanaa.
Kwa mujibu wa BASATA, msanii huyo alikiuka mwongozo huo na kutoheshimu hadhira wakati wa kutumbuiza katika Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava, lililofanyika katika viwanja vya General Tyre jijini Arusha.
Mbali na kutakiwa kulipa faini hiyo, BASATA imemzuia Dudu Baya kujihusisha na shughuli za sanaa kwa namna yoyote hadi atakapotekeleza maamuzi hayo.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni na miongozo inayosimamia maadili na mwenendo wa wasanii wakati wa shughuli za sanaa nchini.