Rais Ruto Kuanza Ziara ya Pwani, Hati Miliki 189,449 Kutolewa
Rais William Ruto anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi katika eneo la Pwani Jumamosi, ambapo atakabidhi takribani hati miliki 189,449 kwa wananchi wa kaunti sita na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ziara hiyo itahusisha kaunti za Taita-Taveta, Kwale, Kilifi, Mombasa, Tana River na Lamu, na itampa Rais fursa ya kukagua maendeleo ya miradi ya Serikali, kuzindua iliyokamilika na kuanzisha mingine mipya. Aidha, atakutana na viongozi pamoja na wananchi kujadili vipaumbele vya maendeleo katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Rais, ugawaji wa hati miliki hizo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kutoa jumla ya hati miliki 500,000 katika eneo la Pwani, hatua inayolenga kutatua changamoto za muda mrefu zinazohusiana na umiliki wa ardhi, zikiwemo migogoro ya ardhi na tatizo la maskwota.
Katika kaunti ya Taita-Taveta, Rais Ruto anatarajiwa kutoa hati miliki 31,318 kwa wakazi wa maeneo ya Mwatate na Voi.
Baadaye, atazuru Kaunti ya Kwale ambako hati miliki 94,175 zitatolewa kwa walengwa katika maeneo bunge ya Lunga Lunga, Msambweni na Kinango.

Kwa upande wa Kilifi, hati miliki 36,826 zinatarajiwa kukabidhiwa kwa wananchi wa maeneo bunge ya Kaloleni, Rabai, Ganze, Kilifi Kusini na Malindi.
Mombasa itapokea hati miliki 4,360, huku hati nyingine 22,770 zikigawiwa kwa wananchi wa kaunti za Lamu na Tana River.
Mbali na suala la ardhi, Rais Ruto pia anatarajiwa kuweka msingi wa ujenzi wa Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Afrika Mashariki (East Africa Refinery) mjini Lamu, mradi mkubwa unaokadiriwa kugharimu takribani dola bilioni 16, sawa na zaidi ya Shilingi trilioni mbili.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Kenya na mfanyabiashara kutoka Nigeria, Aliko Dangote. Kiwanda hicho kinapendekezwa kusafisha mafuta ghafi kutoka Lokichar, Kaunti ya Turkana, na kuzalisha bidhaa za petroli kwa ajili ya masoko ya Afrika Mashariki na Kati.

Serikali inatarajia kuwa kiwanda hicho kitaimarisha usalama wa nishati nchini kwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za petroli, pamoja na kuchochea uwekezaji na kuongeza fursa za ajira.
Katika kipindi cha ziara hiyo, Rais pia anatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali ya miradi ya Serikali, kukagua hatua ya utekelezaji wa miradi inayoendelea na kuzindua miradi mipya katika kaunti zote sita.
Ziara hiyo inatarajiwa kuangazia kwa kiasi kikubwa umiliki wa ardhi, maendeleo ya miundombinu, uwekezaji, nishati na ukuaji wa uchumi katika eneo la Pwani.