Arsenal Yaongeza Kasi Kumnasa Julián Álvarez Kabla ya Pre-Season
Arsenal imeongeza juhudi za kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Julián Álvarez, kabla ya kuanza kwa maandalizi ya msimu mpya, huku kocha Mikel Arteta akimtaja nyota huyo kuwa mmoja wa vipaumbele vyake katika dirisha hili la usajili.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari za usajili Miguel Delaney, viongozi wa Arsenal wanataka dili hilo likamilike mapema ili Álvarez awe sehemu ya kikosi kitakachoanza kambi ya pre-season.

Ripoti hizo pia zinaeleza kuwa mazingira yanaonekana kuipa Arsenal nafasi nzuri ya kumsajili mshambuliaji huyo. Atlético Madrid inadaiwa kutokuwa tayari kumuuza Álvarez kwa klabu yoyote ya La Liga, hatua inayoziondoa timu za Hispania kwenye mbio hizo.
Wakati huo huo, mabingwa wa Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG) wanaelezwa kuwa wameamua kubaki na mshambuliaji wao Bradley Barcola, jambo linalopunguza ushindani katika harakati za Arsenal.
Iwapo mazungumzo yatafanikiwa, Álvarez anatarajiwa kuwa mmoja wa usajili mkubwa wa Arsenal kuelekea msimu wa 2026/27, huku Arteta akilenga kuongeza makali ya safu yake ya ushambuliaji katika mbio za kutwaa mataji.