Mbappé Aahidi Kuitoa Ballon d’Or kwa Afrika Akishinda Tuzo Hiyo

Share this story

Mshambuliaji wa Real Madrid na nahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappé, amesema kuwa bado ana uhusiano mkubwa na mizizi yake ya Afrika, akieleza kuwa upendo anaoupokea kila anapotembelea bara hilo umekuwa wa kipekee.

Mbappé aliyasema hayo katika mahojiano na RFI, akisisitiza kuwa amelelewa katika utamaduni wa Afrika licha ya kuzaliwa na kukulia nchini Ufaransa.

“Sijawahi kukata uhusiano na mizizi yangu na asili yangu. Kila ninapokwenda Afrika, nahisi upendo wa watu na napokelewa kwa furaha kubwa,” alisema Mbappé.

Akizungumzia matumaini yake ya kushinda Ballon d’Or 2026, Mbappé aliwashukuru mashabiki na wadau wa soka barani Afrika kwa sapoti yao, akisema angependa kuihusisha Afrika na mafanikio hayo endapo atatwaa tuzo hiyo.

“Ninawashukuru kwa kila kitu, na ninatumai kuondoka na Ballon d’Or na kwa namna moja au nyingine kuitoa kwa ajili yao pia.”

Mbappé ana mizizi ya Afrika kupitia wazazi wake; baba yake, Wilfried Mbappé, ana asili ya Cameroon, huku mama yake, Fayza Lamari, akiwa na asili ya Algeria. Mbappé pia amewahi kutembelea Cameroon, ambako familia ya upande wa baba yake ina mizizi.

Kauli hiyo imekuja wakati mjadala kuhusu Ballon d’Or 2026 ukiwa umechukua kasi, huku Mbappé akiwa miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo hiyo. Sherehe za utoaji wa tuzo hiyo zimepangwa kufanyika London Oktoba 26, 2026.


Share this story

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Previous post Trump Azindua Kiwanja Kipya cha Helikopta White House