Wachezaji wa Harambee Stars Wagoma Kufanya Mazoezi Wakidai Posho na Maslahi Bora

Share this story

Wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, wamesusia mazoezi kuelekea mechi ya Jumamosi dhidi ya Eritrea katika kuwania kufuzu kwa AFCON 2027, wakidai malipo ya posho na kuboreshwa kwa maslahi yao wanapokuwa katika majukumu ya kitaifa.

Miongoni mwa madai yao ni malazi bora wakati wa mechi za nyumbani na ugenini, usafiri bora wa ndege wenye safari fupi na vituo vichache, pamoja na kulipwa kwa posho zote ambazo bado hazijalipwa. Wachezaji pia wanataka kukutana na Rais William Ruto au viongozi wa Wizara ya Michezo ili kujadili changamoto hizo.

FKF imesema baadhi ya wachezaji wanadai takriban Sh80,000 kila mmoja kutokana na posho za mechi dhidi ya Senegal na Lesotho. Shirikisho hilo limeeleza kuwa jukumu la malipo hayo liko kwa serikali.

Wakati huohuo, kocha wa Harambee Stars Benni McCarthy amefichua kuwa yeye pamoja na baadhi ya wajumbe wa benchi lake la ufundi wamekuwa wakifanya kazi nchini bila vibali vya kazi kwa takriban mwaka mmoja na nusu. McCarthy amesema hali hiyo humlazimu kuondoka Kenya baada ya kumalizika kwa kila kambi ya timu ya taifa na kurejea wakati wa kambi inayofuata.

FKF imesema inashirikiana na serikali kushughulikia suala la vibali vya kazi vya McCarthy na benchi lake. Kuhusu posho, FKF imesema Wizara ya Michezo imeithibitishia kuwa malipo moja yaliyokuwa yakidaiwa kutokana na shughuli ya awali ya Harambee Stars yamekamilishwa na yanatarajiwa kuingia kwa wahusika Alhamisi, huku malipo mengine yakiwa katika hatua mbalimbali za uchakataji.

Harambee Stars wanatarajiwa kuikabili Eritrea Jumamosi, Septemba 26, katika Uwanja wa Nyayo, huku suala la posho na maslahi ya wachezaji likitawala maandalizi ya kikosi.


Share this story

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Previous post Odinga Brother Criticises Uhuru Over Renewed Claims on 2022 Election
Next post BASATA YAMTOZA HARMONIZE FAINI YA SH5 MILIONI