Utendaji wa Kishujaa wa Vozinha Kombe la Dunia Wamfanya Kuvuma Duniani

Josimar Dias maarufu kama Vozinha ameibuka kuwa mmoja wa nyota waliovutia hisia za mashabiki duniani baada ya kiwango chake bora katika 2026 FIFA World Cup kuifanya jina lake kutamba kimataifa.
Kabla ya pambano kubwa dhidi ya Spain, golikipa huyo wa Cape Verde National Football Team alikuwa na takribani wafuasi 50,000 pekee kwenye Instagram. Hata hivyo, baada ya maonyesho yake ya kishujaa katika michuano hiyo, idadi ya wafuasi wake imeongezeka kwa kasi hadi kufikia milioni 2.7.
Mashabiki wengi wa soka duniani wamekuwa wakimsifu Vozinha kwa uchezaji wake wa kujituma, kuokoa michomo muhimu, na kuiongoza Cape Verde kufanya vizuri katika michuano hiyo ya dunia.
Akizungumza kwa hisia kali baada ya mechi, Vozinha alisema alilia kutokana na kukumbuka maisha yake ya utotoni na changamoto alizopitia akiwa mdogo.

“Nimelia kwa sababu wakati nikiwa mtoto nililelewa na babu pamoja na bibi yangu. Nilitamani wawe hapa lakini kwa bahati mbaya walishafariki,” alisema.
Golikipa huyo pia alieleza kuwa mama yake hakuweza kufika kushuhudia mafanikio yake kutokana na changamoto za visa na gharama za usafiri.
“Mama yangu ameshindwa kufika kwa wakati kwa sababu ya masuala ya VISA. Pesa tuliyotakiwa kulipa imefanya VISA isitoke kwa wakati,” aliongeza.
Hadithi ya Vozinha imegusa wengi duniani, huku wengi wakisema kuwa Kombe la Dunia lina uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha ya wachezaji na kuwapa jukwaa la kimataifa ndani ya muda mfupi.