TANZANIA : Vifo 518 Vyathibitishwa Baada ya Ghasia za Uchaguzi Mkuu 2025
Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Oktoba 29, 2026, Othman Chande, amethibitisha kuwa jumla ya watu 518 walipoteza maisha kufuatia ghasia zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akiwasilisha ripoti rasmi mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Jaji Chande alisema kuwa kati ya waliopoteza maisha, wanaume walikuwa 490 sawa na asilimia 94.6, huku wanawake wakiwa 28 ambao ni asilimia 5.4.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa idadi kubwa ya vifo 182, ukifuatiwa na Mwanza (90), Mbeya (80) na Arusha (53).
Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa watoto 21 walikuwa miongoni mwa waliopoteza maisha, ambapo 15 walikuwa na umri kati ya miaka 15 hadi 17, wanne walikuwa na umri wa miaka 7 hadi 10, na wawili walikuwa chini ya miaka mitano.
Kwa upande wa wahanga, Jaji Chande alibainisha kuwa watu 205 walikuwa raia wa kawaida, huku vifo 16 vikihusisha maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Aidha, kuhusu mazingira ya vifo, watu 373 walifikishwa hospitalini wakiwa tayari wamefariki dunia, watu 121 walifariki wakiwa wanapatiwa matibabu, na miili 24 ilipatikana bila taarifa kamili.