Kenya Yapewa Leseni ya Kutengeneza Dawa Mpya ya Kuzuia VVU
Kenya imepewa leseni ya kutengeneza dawa mpya ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa ajili ya soko la Afrika, hatua inayoiweka nchini humo miongoni mwa mataifa ya kwanza barani kushiriki katika uzalishaji wa dawa hiyo.
Dawa hiyo inayojulikana kama Alimatravir, inalenga kutoa kinga dhidi ya maambukizi ya VVU na huenda ikaanza kupatikana katika nchi zinazoendelea iwapo itaonekana kuwa salama na yenye ufanisi.
Hatua hiyo inakuja wakati majaribio ya kitabibu ya dawa hiyo yakitarajiwa kukamilika mwaka ujao. Matokeo ya majaribio hayo ndiyo yatakayoamua iwapo Alimatravir inaweza kuanza kutumika kwa upana.
Leseni hiyo inalenga kuwezesha uzalishaji wa dawa hiyo barani Afrika na kupunguza muda unaohitajika kuifikisha kwa watu wanaohitaji huduma za kinga dhidi ya VVU, endapo itapitishwa kwa matumizi.
Kenya ni miongoni mwa nchi tatu za kwanza barani Afrika kupewa nafasi ya kushiriki katika uzalishaji wa dawa hiyo, hatua inayoweza kuongeza uwezo wa bara hilo katika kutengeneza bidhaa muhimu za afya ndani ya Afrika.