Omar Artan Aweka Historia, Aitwa na UEFA kwa Mafunzo ya Waamuzi
Mwamuzi wa kimataifa kutoka Somalia, Omar Artan Abdulkadir, amepewa nafasi ya kipekee baada ya UEFA kumwalika kushiriki kozi maalum ya mafunzo kwa waamuzi wa kiume itakayofanyika Geneva, Uswisi, kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 2, 2026.
UEFA imewasiliana rasmi na CAF pamoja na Shirikisho la Soka la Somalia kuhusu ushiriki wa Artan katika mafunzo hayo.
Baada ya mafunzo hayo, UEFA pia inapanga kumtumia Artan katika mashindano ya UEFA ya klabu msimu wa 2026/27, jambo linaloweza kumfungulia njia ya kuchezesha mechi za UEFA Champions League.
Iwapo atateuliwa kuchezesha Champions League, Artan ataweka historia ya kuwa miongoni mwa waamuzi wa kwanza kutoka Afrika kusimamia mechi za mashindano hayo, na kuwa mwamuzi wa kwanza kutoka Somalia kufikia hatua hiyo.
Hatua hii ni ishara kubwa ya kuongezeka kwa nafasi ya waamuzi wa Afrika katika mashindano makubwa ya soka barani Ulaya.