Aucho Akaribia Kurejea Kenya, Kenya Police na AFC Leopards Zaanza Vita ya Kumsajili
Kiungo wa kimataifa wa Uganda, Khalid Aucho, anaripotiwa kupokea ofa kutoka kwa klabu mbili za Ligi Kuu ya Kenya (FKF Premier League), Kenya Police FC na AFC Leopards, huku zikisaka huduma zake kuelekea msimu wa 2026/27.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa kwa mara ya kwanza na Mwanaspoti, chanzo cha karibu na nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia kimeeleza kuwa, licha ya kuvutiwa pia na baadhi ya klabu kutoka Saudi Arabia, Aucho anaonekana kuvutiwa zaidi na uwezekano wa kurejea kucheza nchini Kenya.
Iwapo atakubali mojawapo ya ofa hizo, Aucho atarejea katika ligi ambayo aliwahi kung’ara akiwa na Gor Mahia, ambako alijijengea sifa kama mmoja wa viungo bora wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Uamuzi kuhusu mustakabali wa kiungo huyo unatarajiwa kutolewa ndani ya wiki chache zijazo huku klabu zinazomhitaji zikiendelea kusubiri msimamo wake rasmi.
Chanzo: Mwanaspoti Tanzania.