Rais aongoza usambazaji wa fedha za NYOTA Kisii
Rais William Ruto leo ameongoza usambazaji wa fedha kutoka kwa hazina ya NYOTA katika uwanja wa michezo wa Gusii kwa vijana wapatao 8,820, wakazi wa kaunti za Kisii, Nyamira na Migori.
Kwa jumla walengwa katika kaunti hizo wamepokea shilingi milioni 220.5 zitakazowasaidia kuanzisha biashara na kupanua zilizopo.
Vijana hao wamepokea ufadhili huo baada ya kukamilisha kwa mafanikio mafunzo ya lazima ya siku nne ya ujuzi wa biashara.
Mafunzo hayo yaliwapa walionufaika ujuzi wa vitendo katika usimamizi wa fedha, ujasiriamali na ukuzaji wa biashara na hivyo kuwaandaa vyema kuanzisha, kuimarisha na kudumisha biashara zao.
Chini ya awamu ya kwanza ya utoaji wa mtaji wa kuanzisha biashara wa NYOTA, kila mnufaika atapokea shilingi elfu 25.
Elfu 22, zinawekwa moja kwa moja katika akaunti ya Pochi la Biashara ya mnufaika ili kusaidia kuanzisha au kupanua biashara mara moja, huku shilingi elfu 3, zikiwekwa katika akaunti ya akiba kwenye hazina ya NSSF.