Uhuru Kenyatta Aitaka Upinzani Kuungana, Kumtaka Kuteua Mgombea Mmoja wa Urais 2027
Aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amewataka viongozi wa upinzani kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuungana nyuma ya mgombea mmoja wa urais ili kukabiliana na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2027.
Uhuru amesema Wakenya wanahitaji upinzani ulioimarika na wenye umoja, ambao utaweza kutoa ushindani mkubwa dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza katika uchaguzi ujao.
Kauli hiyo aliitoa Jumatano wakati wa ibada ya mazishi ya marehemu binamu yake, Beatrice Wambui Muturi, iliyofanyika katika Kanisa la PCEA Nairobi West jijini Nairobi.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa wa upinzani, akiwemo kiongozi wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Party, Kalonzo Musyoka, pamoja na kiongozi wa DAP-K, Eugene Wamalwa.
Katika hafla hiyo, Uhuru pia alidokeza uwezekano wa kumtembelea Gachagua katika makazi yake ya Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri, ambako aliyekuwa Naibu Rais amekuwa akikutana na viongozi mbalimbali wa upinzani kwa mashauriano kuhusu mikakati ya kumkabili Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027.
Kauli ya Uhuru inaongeza msukumo wa mazungumzo kuhusu uwezekano wa kuunda muungano mpana wa upinzani kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, huku viongozi wa vyama mbalimbali wakitafuta namna ya kushirikiana kisiasa.