ODM Yaondoka Rasmi Azimio, Yafanya Mabadiliko ya Uongozi Bunge la Kaunti ya Nairobi
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimetangaza kujiondoa rasmi katika muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party, huku kikifanya mabadiliko katika nafasi mbalimbali za uongozi wa Bunge la Kaunti ya Nairobi.
Katika mabadiliko hayo, ODM imemteua MCA aliyeteuliwa, Catherine Apiyo Okoth, kuwa mjumbe wa Bodi ya Huduma za Bunge la Kaunti ya Nairobi (Nairobi County Assembly Service Board).
Aidha, MCA wa Upper Savanna, Stazo Omung’ala Elijah Ang’ila, ameteuliwa kuwa Kiranja Mkuu wa Wengi (Majority Whip), akichukua nafasi ya Moses Nyangaresi Ogeto.
Mabadiliko hayo pia yamemshuhudia MCA wa Imara Daima, Evans Okaru Nyangicha, akiteuliwa kuwa Naibu Kiranja Mkuu wa Wengi (Deputy Majority Whip), akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Ang’ila.