Macron, Ruto na Faye Wacheza Mpira Katika Mkutano wa Africa Forward Nairobi
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, alijiunga na Rais wa Kenya, William Ruto, pamoja na Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, katika wakati wa burudani ya mpira wa miguu uliovutia wengi wakati wa Mkutano wa Africa Forward uliofanyika katika University of Nairobi siku ya Jumatatu.
Viongozi hao watatu waliungana na aliyekuwa kocha maarufu wa soka wa Ufaransa, Claude Le Roy, ambapo walionekana wakipigiana pasi chache za mpira katika tukio lililowavutia washiriki wa mkutano huo.
Katika picha na video zilizosambaa mtandaoni, marais hao walionekana wakitabasamu na kufurahia mchezo huo wa kirafiki huku wakijumuika na wageni mbalimbali waliohudhuria mkutano huo mkubwa wa kimataifa.
Tukio hilo lilijiri wakati viongozi hao walipokuwa wakijadili masuala ya biashara ya michezo, uwekezaji kwa vijana, pamoja na nafasi ya michezo katika kukuza uchumi, ajira na diplomasia ya kitamaduni barani Afrika.
Mkutano wa Africa Forward umewakutanisha viongozi mbalimbali kutoka Afrika na mataifa mengine duniani kwa lengo la kujadili mustakabali wa maendeleo ya bara hilo kupitia ushirikiano wa kimataifa, teknolojia, ubunifu na uwekezaji kwa vijana.
