PASTOR EMMANUEL USHINDI WA “DUNDA MU YESU” AFARIKI DUNIA

Huzuni imetanda kufuatia kifo cha Pastor Emmanuel Ushindi, aliyepatikana amefariki katika sehemu aliyokuwa amefikia kulala mjini Bunia, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Pastor Ushindi alikuwa amesafiri kwenda Bunia kuhudhuria mikutano mbalimbali. Baada ya kukamilisha shughuli hizo, alirejea katika eneo alilokuwa amepanga kulala, lakini hakuwahi kuamka tena.
Mwili wake ulipatikana ukiwa na damu iliyotoka puani na uso uliokuwa umevimba, hali iliyosababisha wahudumu wa afya wanaohusika na masuala ya Ebola kuitwa ili kushughulikia mwili huo kwa tahadhari.

Hata hivyo, hakuna uthibitisho uliotolewa kuhusu chanzo cha kifo chake wala iwapo kilihusiana na Ebola. Uchunguzi zaidi unahitajika kubaini mazingira na sababu za kifo hicho.
Kifo cha Pastor Ushindi kimewaacha familia yake, marafiki na waumini katika majonzi, huku wengi wakituma salamu za rambirambi na pole kwa wote walioathiriwa na msiba huo.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi na awape wafiwa nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.