Wimbo Wa ‘Mtasubiri’ Wa Diamond Na Zuchu Wapigwa Marufuku Tanzania
Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) iliipiga marufuku video ya Diamond aliyomshirikisha Zuchu ya “Mtasubiri” kufuatia malalamishi ya baadhi ya waumini wa madhebehu ya dini nchini humo.
Kikundi cha waumini kiliwasilisha ombi la kufutwa kwa video hiyo wakidai kuwa kuna kipande ambacho kinaashiria dharau kwa dini ya kikristu.
“Msanii tajwa (Diamond Platnumz) ametoa video ya wimbo unaofahamika kama ‘Mtasubiri Sana’ na katika video hiyo kuna kipande kimeonyesha wahusika wapo kanisani wanaimba kwaya lakini baadae wakaacha na kuelekea kwingine. Kipande hicho cha video kimeleta ukakasi miongoni mwa waumini wa madhebehu ya dini na kuleta hisia kwamba ni dharau ya dini/madhebehu fulani,” Taarifa iliyopigwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA Dkt Jabiri K. Bakari ilisoma.
Agizo la TCRA lilitoka baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwamba video ya wimbo huo imekwaza waumini fulani. Vyombo vya habari nchini Tanzania viliagizwa visicheze video ya wimbo “Mtasubiri” hadi pale wanamuziki hao wawili wa WCB Wasafi wairekebishe na kutoa sehemu hiyo inayoudhi kwenye video hiyo.
Video hiyo iliyotoka mwezi mmoja uliopita mpaka sasa imeshatazamwa na watu zaidi ya milioni 10 kwenye mtandao wa Youtube na ni moja kati ya nyimbo zilizoko katika albamu fupi (EP) ya First of All (FOA) ukiwa wimbo namba nne.