Wasiwasi kuhusu viwanja maafisa wa CAF wakianza ziara Jumatano
Wasiwasi umejaa Kenya kuwa huenda ikapoteza nafasi ya kuandaa michuano ya CHAN mwaka ujao kutokana na uzembe wa ujenzi kwenye viwanja vilivyopendekezwa kwa mechi hizo za wachezaji wanaosakata soka kwenye ligi za nyumbani.
Kenya pamoja na mataifa jirani — Uganda na Tanzania zimepewa fursa ya kuandaa kwa pamoja michuano hiyo, lakini kuna hofu kwamba ujumbe wa CAF unaozuru nchini kuanzia Jumatano, Novemba 27, 2024 utapata kama haviko tayari.
Mbali na mashindano hayo yaliyotarajiwa kufanyika mwaka huu, vile vile mataifa hayo ya Afrika Mashariki yamepewa idhini kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za 2027.
Kulingana na Kamati ya Kitaifa ya maandalizi ya michuano ya CHAN, ujumbe wa CAF utawasili nchini Jumatano kufanya ukaguzi wake wa pili kwenye viwanja pamoja na vifaa vingine muhimu na kumaliza shughuli hizo mwishoni mwa wiki.
Ujumbe huu unawasili wakati Kenya iko mbioni kutayarisha viwanja vya Nyayo na Kasarani na Talanta Sports Center vilivypendekezwa kwa michuano hiyo kuhakikisha vinafikia viwango vya kimataifa kulingana na matakwa ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).
Mbali na viwanja, ujumbe huo utakagua hoteli, viwanja vya ndege, viwanja vya mazoezi miongoni mwa vifaa vingine muhimu. Huu ni ukaguzi wa pili kufanyiwa mataifa hayo wenyeji baada mwingine ulioongozwa na rais wa CAF, Patrice Motsepe kufanyika Septemba, 2024 na kutoa ripoti kwamba uliridhika na maandalizi ya Uganda na Tanzania.
Ujumbe unaozuru nchini unajumuisha maarifa wa CAF kutoka idara ya masoko, mawasiliano, utangazaji, ushindani, usalama wa matibabu itifaki.
Majuzi, ukosefu wa viwanja vya kimataifa nchini ulisababisha kuahirishwa kwa mechi kubwa kati ya AFC Leopards na Gor Mahia maarufu kama Mashemeji Derby iliyoratibiwa kuchezewa Nyayo Stadium, Novemba 24.
Nyayo Stadium ulio na uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 30,000 unafanyiwa marekebisho yanayotarajiwa kumalizika mwezi ujao kwa ajili ya uandalizi wa michuano ya CHAN.