Wasanii Wa Bongo Fleva, Killy Na Cheed Wajiondoa Rasmi Kwenye Lebo Ya Konde Gang
Lebo ya Konde Music Worldwide inayomilikiwa na mwimbaji na mtunzi wa nyimbo, Harmonize, leo tarehe October 10, 2022 imetangaza rasmi kuwa Killy na Cheed hawapo tena chini ya uongozi wa lebo hiyo. Tangazo hilo limekuja siku chache tangu Harmonize adokeze kuwa anakaribia kusajili wasanii wawili wapya kwenye lebo yake.
Uongozi wa Konde Music Wordwide umetangaza kuagana na kusitisha mikataba ya Wasanii Ally Kili Omary (Killy) na Rashid Daudi Manga (Cheed) kwasababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo Konde Music.
“Wasanii hawa watakuwa Wasanii huru na kufanya kazi na kuingia mkataba na Kundi au Mtu yeyote na kuendeleza kazi zao kwakuwa tunaamini ni Vijana Wasanii wenye uwezo mkubwa wa kufanikiwa katika safari ya muziki” Taarifa rasmi ya Konde Gang
“Aidha, Konde Music Worldwide haitahusika na jambo lolote litakalohusisha Wasanii hawa kuanzia leo, tunapenda kuwashukuru Killy na Cheed Kwa ushirikiano wao katika kipindi chote cha kuwa pamoja na tunawatakia mafaniko mema katika kazi zao hapo baadaye”
Wasanii hao wawili bado hawajatoa taarifa rasmi juu ya kuondoka kwao lakini hadi sasa wameondoa Saini ya Konde Gang kwenye bio zao za Instagram huku Cheed akienda mbali zaidi kufuta posti zote kwenye akaunti yake.
Cheed na Killy walijiunga na Konde Gang mnamo 2020 na hapo awali walikuwa sehemu ya Ali Kiba, label ya Kings Music. Mbali na Cheed na Killy, Country Wizzy ni msanii mwingine ambaye hivi karibuni ameachana na kundi la Konde Gang na kuamua kujitegemea. Mpaka sasa Skales, Harmonize, Ibraah, na Anjella ndio wasanii pekee waliochini ya label hiyo.