Mary Moraa anyakua medali ya shaba katika mbio za mita 800
Mary Moraa ambaye alikuwa Mkenya pekee katika fainali ya mita 800 kwa wanawake aliibuka wa tatu na kunyakua medali ya shaba katika Olimpiki ya Paris 2024 Jumatatu usiku.
Moraa alikuwa akitarajia kutoa Kenya katika ukame wa medali ya dhahabu kwenye Olimpiki tangu mwaka wa 2008 Pamela Chelimo aliposhinda kule Beijing China. Wakati huo Janet Chepkosgey alishinda fedha.
Bingwa huyo wa dunia mwaka wa 2023 alikuwa karibu kunyakua medali hiyo huku kukiwa kumebakia mita 200 akiwa mbele unyo kwa unyo na Keely Hodgkinson wa Great Britain.
Hata hivyo Hodgkinson alimlemea mwisho mwisho na kuongoza huku Moraa akijipata wa tatu baada ya Mhabeshi Tsige Duguma kumpiku hatua chache kabla ya utepeni.
Hodgkinson alitumia muda wa dakika 1:56.72 kunyakua dhahabu. Duguma alitimka kwa dakika 1:57.15 kujishindia nishani ya fedha. Moraa alitumia muda wa dakika 1:57.42 kunyakua shaba.