Kesi Dhidi Ya Platini Na Blatter Kuanza Yaendelea

Share this story

Aliyekuwa rais wa FIFA, Sepp Blatter, na gwiji wa soka wa Ufaransa, Michel Platini, wamefika tena mahakamani nchini Uswisi kujibu mashtaka ya ubadhirifu.

Mnamo 2022, wawili hao waliondolewa hatiani katika kesi iliyohusu malipo ya faranga milioni 2 za Uswisi (£1.6m) yaliyotolewa kwa Platini kwa idhini ya Blatter mnamo 2011.

Blatter, mwenye umri wa miaka 88, alisisitiza kuwa hana hatia, akisema: “Unapozungumzia uongo na udanganyifu, hilo halinihusu. Katika maisha yangu yote, hilo halijawahi kuwepo.”

Hata hivyo, mwendesha mashtaka wa shirikisho la Uswisi alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo, na kesi mpya inatarajiwa kuendelea hadi Alhamisi, huku hukumu ikitarajiwa kutolewa tarehe 25 Machi.

Platini, mwenye umri wa miaka 69, aliyewahi kuwa rais wa UEFA, alihusika katika soka kwa mafanikio makubwa, akishinda tuzo ya Ballon d’Or mara tatu na kuiongoza Ufaransa kutwaa ubingwa wa Euro 1984.

Mnamo 2015, Blatter na Platini walifungiwa kujihusisha na soka kutokana na ukiukwaji wa maadili ya FIFA, huku mashtaka ya udanganyifu na kughushi yakifunguliwa dhidi yao.

Katika kesi ya kwanza, walidai kuwa malipo hayo yalikuwa ni sehemu ya makubaliano ya awali ya kazi ya ushauri kwa Platini, ambayo FIFA ilichelewa kumlipa kutokana na ukata wa kifedha.

Mahakama ya rufaa mjini Muttenz, karibu na Basel, sasa itatoa uamuzi wa mwisho kuhusu kesi hii yenye utata.


Share this story

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Previous post Aliyependekeza Jina La Tanzania Aaga Dunia