Julian Alvarez ajiunga na Atletico Madrid
Mshambulizi wa Manchester City Julian Alvarez amesajiliwa na klabu ya Atletico Madrid kwa mkataba wa miaka sita kwa thamani ya pesa kiasi cha £81.5 milioni.
Mwajentina huyo kwenye umri wa miaka 24 amekuja kuchukua nafasi ya Alvaro Morata aliyehamia AC Milan inayoshiriki ligi ya Serie A.
Anaondoka City akiwa ameshiriki mechi 103 katika mashindano yote akifunga mabao 36 tangu ajiunge nao kutoka River Plate ya Argentina mwaka wa 2022.
Amefanikiwa kushinda mataji mawili ya Ligi ya Premia, moja ya Kombe la FA, moja ya Ligi ya Mabingwa bara Ulaya, moja ya Kombe la Dunia kwa Vilabu na moja ya UEFA Super Cup.
Katika msimu wa 2023/24, Alvarez alifunga mabao 19 katika mashindano yote kwa mechi 54. Bao lake la mwisho kwenye ligi ya EPL lilikuwa dhidi ya Fulham uwanjani Craven Cottage ambapo City iliibuka na ushindi wa 4 – 0 mnamo Mei 11.
Alvarez amechezea timu ya taifa ya Argentina tangu mwaka wa 2021. Alishirikishwa kwenye kikosi kilichoshiriki mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2022.
Aliwakilisha taifa lake kwenye Kombe la Dunia akifunga mabao manne na kusaidia taifa lake kushinda Kombe la Dunia. Pia alisaidia taifa lake kushinda taji la Copa America mwaka wa 2024.
Alvarez alishirikishwa kwenye kikosi kilichoshiriki Olimpiki ya Paris 2024. Alicheza mechi nne huku akipeana usaidizi mara mbili. Hata hivyo, timu ya Argentina ilibanduliwa nje kwenye hatua ya robo fainali na Ufaransa.