Cheruiyot na Komen kurejesha nyota ya Kenya kwenye mita 1500
Timothy Cheruiyot na Brian Komen wako mbioni leo Jumanne usiku wataingia uwanjani kwenye fainali ya mita 1,500 kwa wanaume katika Olimpiki ya Paris 2024.
Wawili hao wanatarajiwa kurejesha nyota ya Kenya ambayo imezimwa tangu mwaka wa 2008 katika Olimpiki ya Beijing nchini China. Asbel Kiprop alinyakua dhahabu na tangu hapo imekuwa ndoto.
Bingwa mtetezi ni Jakob Ingebrigsten wa Norway ambaye alishinda katika Olimpiki ya Tokyo 2020. Cheruiyot alikuwa wa pili. Naye Josh Kerr wa Great Britain alimaliza wa tatu.
Kenya wana upinzani kutoka Ingebrigsten na Kerr kulingana na fomu yao.
Cheruiyot karibu akose kufuzu fainali baada ya kukimbia kwenye mstari wa ndani katika muda wote wa mbio hizo kabla ya kuamua kutoka nje na kujinusuru akimaliza wanne.
Akitumia mbinu hiyo atajipata pabaya. Mwenzake Komen alitumia mbuni hiyo kabla ya kujiondoa kwenye kundi na kuongeza kasi na kufuzu. Yeye ni bingwa wa bara Afrika. Ni mara ya kwanza kwa Komen kushiriki Olimpiki. Mbio hizo zitaanza mnamo saa tatu na dakika hamsini (9:50 pm EAT)