
Ancelotti Ateuliwa Kuwa Kocha Wa Timu Ya Taifa Ya Brazil
SHIRIKISHO la soka Nchini Brazil (CBF) limethibitisha kumteua kocha Muitaliano Carlo Ancelotti kuwa kocha mkuu mpya wa Mabingwa hao mara 5 wa kombe la Dunia la FIFA na kuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuinoa timu hiyo tangu mwaka 1925.
Ancelotti (65) ambaye anatarajiwa kuondoka Real Madrid baada ya kutamatika kwa msimu wa Ligi Kuu Uhispania huku nafasi yake ikichukuliwa na Xabi Alonso klabuni hapo alishuhudia Real Madrid ikipoteza mechi nne mfululizo msimu huu dhidi ya Hanci Flick na vijana wake wa Barcelona kufuatia kipigo cha 4-3 kwenye ‘El Classico’ ya mwisho siku ya Jumapili.
Muitaliano huyo ambaye amewahi kuvinoa vilabu vya AC Milan, Chelsea, Real Madrid na Paris Saint-German ataanza kazi yake hiyo mpya Mei 26, 2025 siku moja baada ya Real Madrid kucheza mechi yao ya mwisho ya ligi msimu huu dhidi ya Real Sociedad.
Katika taarifa yake, CBF imemsifu Mshindi huyo mara 7 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (mara 5 kama kocha na mara 2 kama mchezaji) likimtaja Ancelotti kama Gwiji wa soka ambaye ana rekodi ya ajabu katika soka la Ulaya na kuelezea matumaini ya zama mpya kwa Brazil zenye mafanikio chini ya uongozi wake.
“Ancelotti ni gwiji wa mchezo wa soka kama meneja aliyefanikiwa zaidi katika historia ya soka, atachukua jukumu rasmi baada ya kumalizika kwa msimu wa 2024/25 wa La Liga, kabla ya kampeni ya Brazil ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA mnamo Juni. Tarehe yake ya kuanza rasmi Mei 26, 2025.” — imesema taarifa ya CBF kuhusu kocha ambaye pia amewahi kuvinoa vilabu vya AC Parma, Juventus, Napoli na Everton.