Wabunge wa Pwani wanadai haki kwa mzee aliyeuawa na afisa wa KWS
KUNDI la Wabunge wa Pwani (CPG) limeitaka Wizara ya Utalii na Wanyamapori kuharakisha uundaji wa korido ya malisho katika Kijiji cha Yakaliche, Jimbo la Garsen, ili kukabiliana na mgogoro unaoendelea kati ya binadamu na wanyamapori katika eneo hilo.
Wabunge hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CPG na Mbunge wa Matuga Kassim Tandaza, waliandamana hadi afisi za Shirika la Huduma za Wanyamapori (KWS) Kanda ya Pwani (KWS) mjini Mombasa kuwasilisha barua ya maandamano.
Hii ilifuatia mauaji ya mzee, Issack Jarso Delo, yanayodaiwa kufanywa na afisa wa KWS mnamo Desemba 29, 2024. Kulingana na maelezo ya walioshuhudia, mzee huyo aliuawa katika boma lake mbele ya familia yake, kinyume na madai ya KWS kwamba kisa hicho kilitokea katika Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo Mashariki.
Wabunge hao walilaumu mzozo unaoongezeka kutokana na ukosefu wa korido maalumu kwa ajili ya wafugaji kupata malisho na maji ndani ya hifadhi hiyo. Waliitaka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuharakisha uchunguzi na kumshtaki afisa aliyehusika. Zaidi ya hayo, walitaka KWS kufidia familia ya marehemu.