GOVERNOR ANDREW MWADIME SPEECH DURING MASHUJAA DAY CELEBRATIONS

Share this story

Naibu Gavana……..

Mkuu wa Kaunti

Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Kitaifa,

Mheshimiwa Wabunge wa Seneti,

Mheshimiwa Muwakilishi wa kina mama

Spika wa Bunge la Kaunti,

Katibu wa Kaunti

Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Kaunti,

Washauri katika Afisi yangu,

Maafisa wakuu wa wizara mbalimbali,

Viongozi wa Serikali ya Kitaifa,

Wajumbe wa Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti,

Maafisa wengine wa serikali ya kaunti,

Washirika wetu wa Maendeleo,

Wageni Waalikwa,

Waandishi wa habari,

Mabibi na mabwana,

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa neema ya kuona siku hii tuliyotamani kuiona. Naomba vilevile, nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi wote wa Taita Taveta kwa kunichagua kama gavana wenu wa Tatu wa jimbo hili tunalo lipenda.

Sherehe hii ya muhimu inaidhinisha na kukumbuka kujitolea kwa waanzilishi wa Taifa letu la Kenya kama vile Mzee Jomo Kenyatta, Bildad Kaggia, Achieng’ Oneko, Paul Ngei na wengineo ambao walipambana na kumwondoa Mbeberu na Mkoloni na kutuletea Uhuru tunaoufurahia hadi kufikia sasa. Hapa kwetu Taita Taveta, tunajivunia mashujaa kama vile Mwangeka wa Malowa, Dawson Mwanyumba, Eliud Mwamunga, Frank Dingiria, Tsighoi Mcharo na hata Mashujaa wa sasa kama vile Meja Mstaafu Marsden Madoka, Mashengu wa Mwachofi, mwanariadha Phanuel Mkungo, na wengineo.

Na kwa njia ya kipekee, Tujumuike Pamoja kusherehekea vijana wetu wa Dr Aggrey Boys High School kwa kupeperusha jina la Kaunti hii na Kenya nzima.

Na mwisho kabisa, niwasherehekee wananchi wote wa Kaunti ya Taita Taveta kwa bidii mnayofanya kuikuza Kaunti yetu,

nyinyi nyote ni Mashujaa!!!!

Mabibi na Mabwana

Katika kampeni za kuomba kura zenu, niliahidi mambo kadhaa wa kadha. Tumeingia mwezi wa pili tangu nichukue hatamuza uongozi wa Kaunti hii. Nina furaha kuwatangazia leo ya kwamba tayari tumeanza kuona matunda ya kazi yetu.

Tumeweza kulipa malimbikizi yote ya mishahara ya wafanyi kazi wote wa Kaunti

Tumeweza kulipa wafanyi kazi waliosimamishwa kazi miaka ya hapo mbeleni

Tumepata fidia ya wahanga wa migogoro ya binadamu na wanyamapori

Tumeanza kuboresha mifumo ya huduma za afya

Tumeweka mikakati ya kuhakikisha usawa wa kijinsia

Tumeweka mikakati ya kuhifadhi mazingira kuboresha viwango vya elimu, na

Tumekuza ushirikiano na wawekezaji kutoka hapa nchini na kutoka nchi za nje

Napenda kuwahakikishia wafanya kazi wa Kaunti na wananchi wote ya kwamba kutoka sasa, mishahara yao haitachelewa tena.

Mambo sasa yamebadilika. Na sitachoka kurudia tena : MAMBO SASA YAMEBADILIKA !!!

Tutajenga Kaunti hii kwa AMANI, UPENDO NA MAENDELEO !!

Mabibi na mabwana,

Kama vile mnafahamu kuwa mimi ndiye mwenyekiti wa kamati ya Maji, Misitu na Usimamizi wa Maliasili katika baraza la magavana, hivyo nitajitahidi kuhifadhi mazingira katika mtindo wa kunufaisha mwananchi.

Kuhusiana na hili, utawala wangu tayari umeshirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kukamilisha uondoaji wa mchanga kwa bwawa la Manoa.

Zoezi hili limekamilika wakati muafaka kabla ya mvua zinazotarajiwa kunyesha miezi ya Oktoba, Novemba na Disemba.

Mradi huu umekamilika mwezi mmoja baada ya kutoa ahadi ya kutekeleza zoezi hili lililowekwa ili kuongeza uwezo wa miundombinu ya kusambaza maji kwa wakazi wa maeneo hayo kwa matumizi ya nyumbani na kilimo.

Familia 200 zimelengwa ili kufaidika.

Ukarabati wa mara kwa mara wa mabwawa na vyanzo vya maji ni mojawapo wa ajenda zangu. Mikakati hii inalenga kuhakikisha kupunguza hali ya uhaba wa maji unaochangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanasababisha misimu mirefu ya ukame.

Mabibi na mabwana,

Nimekutana na wahifadhi ambao wanataka kupeana matokeo ya suluhisho utekelezaji wa sera zilizoko, na kuhakikisha urejeshaji na upandaji wa misitu katika mandhari ya kaunti ya Taita Taveta.

Hii itakuwa kupitia kuwezesha urejeshaji wa mashamba, misitu na ardhi ya malisho katika kaunti yetu iliyojaliwa vyema na raslimali.

Uwekezaji huu utakuza uhifadhi wa mazingira ya kaunti katika mfumo endelevu, jinsi ilivyoratibiwa na malengo ya maendeleo endelevu maarufu kama SDGs.

Mwongozo huo wa kimataifa unalenga kusimamia misitu kwa njia endelevu, kukabiliana na kuenea kwa jangwa, kusimamisha na kurudisha nyuma uharibifu wa ardhi na kukomesha upotevu wa mimea na wanyama.

Natumaini kwamba kwa ushirikiano huu tutajenga mabwawa katika maeneo ya nyanda za juu na mandhari ya milima ambayo inaungana na maeneo ya mabondeni ili kujenga vyanzo vya maji kwa ajili ya kilimo.

Mabwawa hayo yatadhibiti kasi ya maji, kuhifadhi udongo, na kuboresha ardhi.

Ardhi lazima iboreshwe kwa kurudisha nyuma uharibifu wa ardhi, kurudisha nyuma athari za mabadiliko ya hali ya hewa, uhaba wa chakula na lishe, na kuboresha mimea na wanyama.

Suluhu hizi zinatokana na matokeo ya utafiti yaliyokusanywa kutokana na mawaidha na mahitaji ya watu.

Mradi huu unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni utafanyika katika kaunti ya Taita Taveta na Makueni.

Kumbuka kuwa manifesto yangu inahusu kukuza uhifadhi wa mazingira katika mfumo endelevu.

Kwa hiyo, utawala wangu utashirikiana na wafadhili na wawekezaji wengi zaidi, wakiwemo wale ambao wamekuwa wakitusaidia kama vile Benki ya Dunia, na Shirika la Msalaba Mwekundu pamoja na mashirika mengine, ili kujenga mabwawa makubwa, kukarabati na kuangua mabwawa hayo ikiwemo mabwawa ya Kighombo, Kishenyi, Mwatate na mengineyo. Hii ni pamoja na kukamilisha miradi ya maji iliyokwama. Juhudi zetu pia zitazingatia uvunaji wa maji ya mvua katika kila nyumba na ukarabati wa vyanzo vya maji.

USAWA WA KIJINSIA NA UWEZESHAJI NA HUDUMA ZA KIJAMII

Mabibi na mabwana,

Mwezi Oktoba pekee, Kaunti ya Taita Taveta iliandaa hafla mbili za kimataifa : Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike iliyofanyika tarehe 12 Oktoba na Siku ya Kimataifa ya Mwanamke wa Kijijini iliyofanyika tarehe 15 Oktoba.

Hii ni mara ya kwanza kila moja ya siku hizi za kimataifa zilizotangazwa na Umoja wa Mataifa kufanyika katika Kaunti ya Taita Taveta.

Katika Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike iliyofanyika Taveta chini ya kaulimbiu: Wakati wetu ni sasa, haki zetu, mustakabali wetu, timu yangu, washirika na wazee kutoka Kenya na Tanzania walikaa kuleta suluhu la suala la watoto wa kike kuvuka mpaka ili wapashwe tohara.

Tukishirikia na Serikali kuu, tumefaulu kuweka mikakati ya kukomesha ukeketaji katika Kaunti hii.

Katika Siku ya Kimataifa ya Mwanamke anayeishi Mashambani iliyofanyika Kishushe, Kaunti ya Taita Taveta ilikaribisha zaidi ya wanawake 600 kutoka kaunti za Siaya, Homabay, Kakamega, Busia, Baringo, Tana River, Kiambu, Mombasa, Kwale, Kilifi, na Nairobi.

Ilikuwa ni furaha kwa utawala wangu kushirikiana na washirika kama vile Actionaid Actionaid, Shirika la Chakula na Kilimo FAO, Groots Kenya, Daughters of Mumbi Resource Centre, Sauti Ya Wanawake, na RECONCILE kufanya siku hii iwe ya kufana na pia kusaidia wanawake na wasichana wa vijijini, ili kuwajengea uwezo, ujuzi na uongozi.

Akina mama, barikiweni sana!!

ELIMU

Mabibi na mabwana

Serikali yangu kwa nia ya kuboresha viwango vya elimu na iliondoa malimbikizo ya thamani ya Shillingi millioni 15 ikiwalenga wanafunzi 400 ambao walikuwa wamefaidika na mpango wa ufadhili wa masomo ya sekondari ya kaunti.

Hatua hii ilikuwa kuhakikisha maendeleo mazuri ya wanafunzi na kuwezesha mpito katika vyuo vya elimu ya juu.

La kukumbukwa ni kwamba manifesto yangu inazungumza kuhusu kutengeneza jamii iliyoelimika vyema.

Hali hii pia inalingana na lengo 4 la maendeleo endelevu linalotetea mafunzo ya maisha yote ya binadamu.

Katika siku chache za hatamu ya uongozi wangu, nimehakikisha kwamba, serikali yangu ina anza mchakato wa kutafutia taasisi zetu za kiserikali hati miliki za ardhi, ambapo Chuo kikuu cha Taita Taveta tayari kimepata hati hiyo na sasa kitaweza kupata ufadhili wa maendeleo.

Kama nilivyosema katika hotuba zangu, nimeweka wazi mlango kwa wawekezaji na wafadhili ili tufanye kazi pamoja tujenge Taita Taveta yetu.

Nimetenga ofisi, iliyo karibu na ofsi yangu ya kuhakikisha wawekezaji wanakaribishwa na kufanyiwa ufuatiliaji ifaavyo, na kwamba wanapewa mazingira mazuri ya utendaji kazi.

Nina karibisha yeyote yule aliye na wafadhili, wawekezaji, washirika wa maendeleo waje katika kaunti hii,tuweze kuungana Pamoja na kutatua maswala kadha wa kadha yanayo kumba wakaazi wa kaunti ya Taita Taveta.

Mengi yametokea hadi sasa.

Mengi yako njiani.

Mabibi na mabwana,

Kama nilivyosema awali katika hotuba zilizopita, najitahidi kuunda miundo sahihi katika serikali yangu ili kuhakikisha usanifu wa ugatuzi una manufaa kwa kila mtu hasa wale walio katika ngazi ya chini.

Nitahakikisha kwamba mwananchi ana husishwa katika ushiriki wa umma, na kutoa maamuzi yatakayo mfaa yeye, na maamuzi hayo kutekelezwa.

Ningependi kuwasihi, mjitokeze kwa wingi pale mnapoitwa kutoa maoni hasa tunapoenda kufanya mpango wa maendeleo ya Kaunti ya miaka mitano ijayo,mipango hii ndio itakayotuongoza katika maendeleo tuitakayoweza kutekeleza katika kipindi cha uongozi wangu wa kaunti.

Hivi Karibuni, nitatoa ratiba ya nitakavyo tembelea Kaunti ndogo za Taveta, Wundanyi na Voi, ili kusikiliza hoja na mapendekezo yao.Nitatembea nyanjani na pia kuhakikisha ofisi zangu katika maeneo haya, zinafanya kazi.

Mabibi na Mabwana,nimefanya teuzi kadhaa, hivi karibuni zaidi ni nyadhifa za wajumbe wakuu.

Nachukua fursa hii kuwafahamisha kuwa niliowachagua nilizingatia utimilifu wa katiba, ushirikishwaji, utofauti, weledi, na uzoefu.

Kwa mawaziri 10 ambao nimewateua, mtapigwa msasa katika Bunge la Kaunti, ambapo ninawatakia kila la heri.

Nikimalizia,

Mabibi na mabwana,

Ninaomba tuendelee kustawisha uhusiano wetu wa ushirikiano kwa manufaa bora ya Kaunti ya Taita Taveta.

Kwa pamoja tutafanikiwa kama mashujaa tuliokusudiwa kuwa.

Sisi sote tuwe mashujaa wa amani, upendo na maendeleo.

Mungu na aibariki Kaunti ya Taita Taveta!

Mungu ibariki Kenya!


Share this story

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Previous post How Indians Dance In Weddings
Next post