Cha Matasi Bado Kimotoni
Mahakama Kuu ya Kakamega imeipa FKF ruhusa kuendelea na mchakato wa kinidhamu dhidi ya kipa wa zamani Patrick Matasi, baada ya kutupilia mbali kesi aliyowasilisha kupinga kusimamishwa kwake. FKF imesisitiza itaendeleza uchunguzi kuhakikisha uadilifu katika soka.
Matasi alisimamishwa na FKF kwa kipindi cha siku 90 kufuatia kuenea kwa video inayodaiwa kumuonyesha akiwa ndani ya gari akijadili mipango ya kupanga matokeo ya mchezo usiofahamika.
Mnamo Aprili 8, 2025, Matasi alipata amri za muda za mahakama zilizozuia FKF kutekeleza kusimamishwa kwake hadi uchunguzi zaidi utakapokamilika.
Hata hivyo, katika kufuta amri hizo, mahakama ilikubaliana na hoja za FKF na kubaini kuwa shirikisho hilo lilifuata taratibu na kanuni zake ipasavyo. Uamuzi huo ni nafuu kubwa kwa FKF katika juhudi zake za kutekeleza Kanuni za FKF za Kupambana na Upangaji Matokeo (FKF Anti–Match Manipulation Regulations).
FKF iliwakilishwa kwenye shauri hilo na kampuni ya mawakili ya Ochutsi Munyendo and Company Advocates.