Cha Mackenzie Bado Jikoni, Mahakama Yakataa Kumwachilia Kwa Dhamana
Mahakama ya Mombasa imekataa kutoa dhamana kwa kiongozi wa kidini Paul Mackenzie pamoja na wazazi 38 wa watoto waliookolewa kutoka msitu wa Shakahola, kwa sababu ya kuingiliwa kwa mashahidi.
Wakili wa washukiwa hao Wycliffe Makasembo aliwasilisha ombi la mdomo kutaka washtakiwa wote waachiliwe kwa dhamana. Hata hivyo, maombi hayo yalipingwa na upande wa mashtaka ambao uliwasilisha hati ya kiapo kuunga mkono kunyimwa dhamana.
Uamuzi huo ulitolewa na kutiwa saini na hakimu mkuu wa mahakama ya Tononoka Nelly Chepchirchi ambaye aliwanyima dhamana washtakiwa.
“Baada ya kuzingatia aina ya makosa ambayo washtakiwa wanashitakiwa nayo na haja ya kulinda maslahi ya watoto ambao ni mashahidi katika suala hili, na ambao mshtakiwa anaweza au ana mamlaka juu yake, naona kuwa hizi ni sababu za msingi kwa inawataka washtakiwa wote kunyimwa dhamana wakati huu,” alisema.
Mipangilio ya kesi hiyo imepangwa kufanyika Aprili 23.