Mahakama Yasitisha Gachagua Kuondolewa Umakamo wa Rais Kenya
Mahakama Kuu Nchini Kenya imesitisha kwa muda utekelezwaji wa azimio la Seneti la kuidhinisha mashtaka ya kumuondoa madarakani, Naibu Rais, Rigathi Gachagua.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji E.C. Mwita ambapo mbali na kuzuia kutekelezwa kwa azimio hilo la Seneti, umezuia pia Rais kumteua Mtu mwingine kuichukua nafasi hiyo hadi October 24,2024 kesi hiyo itakaposikilizwa na Jopo la Majaji watakaoteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Hata hivyo haya yanajiri wakati tayari Rais wa Kenya, William Ruto akiwa amemteua Waziri wa Usalama wa Ndani, Profesa Kithure Kindiki kuichukua nafasi ya Gachagua na Bunge la Taifa limeafiki uteuzi wake.
Itakumbukwa Maseneta Nchini humo waliidhinisha mashtaka 5 kati ya 11 dhidi ya Gachagua na kumuondoa ofisini, Gachagua alishindwa kufika mbele ya Maseneta kujitetea baada ya Mawakili wake kusema alipatwa na maumivu makali ya kifua na kulazimika kulazwa Hospitalini.