EACC imewakamata maafisa 4 Taita Taveta
Ofisi ya mwongoza mashtaka ya DPP ameidhinisha mashtaka ya ufisadi dhidi ya maafisa wanne wa Kaunti ya Taita Taveta akiwemo mshauri wa masuala ya kiuchumi wa gavana na aliyekuwa katibu wa kaunti hiyo.
Maafisa wanne wakuu wa Kaunti ya Taita Taveta waliokamatwa Jumanne kwa madai ya wizi wa pesa za umma Ksh.7 milioni kwa kisingizio cha kuadhimisha Vita vya Kwanza vya Dunia wanafikishwa mahakamani Jumatano. Thomas Jumwa, Mshauri wa sasa wa Uchumi wa Gavana Andrew Mwadime; aliyekuwa Katibu wa Kaunti, Liverson Mghendi; aliyekuwa Afisa Mkuu wa Fedha Leonard Langat; na Christine Wakera, afisa mkuu wa zamani wa Biashara, Utalii na Maendeleo ya Ushirika, walikamatwa na makachero wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Mombasa Central.
EACC ilisema watashtakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi, kughushi, kujihusisha na mradi bila mipango ya awali, kula njama ya kutenda kosa la ufisadi, na kutoa hati za uwongo kinyume na sheria.
Wanne hao walifikishwa mbele ya Mahakama ya Kupambana na Ufisadi Mombasa na baadaye wakaachiliwa kwa dhamana.