
RAISI RUTO ARUSHIWA KIATU AKIWA ZIARA YA KAZI.
Serikali ya Kenya imeelezea tukio la kurushiwa kiatu kwa Rais William Ruto kama la “aibu” na lisilokubalika, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Jumapili.
Video zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zinaonyesha kiatu kikimgonga rais kwenye mkono wa kushoto alipokuwa ameuinua juu akizungumza.
Msemaji wa serikali, Isaac Mwaura, alilaani tukio hilo na kuitaka mamlaka husika kuwakamata waliohusika.
“Je, nini kingetokea kama sote tungeamua kurushiana viatu? Ni maadili gani tunayowafundisha watoto wetu?” alihoji kupitia chapisho lake katika mtandao wa X, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu taasisi ya urais.
Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kuwa watu watatu wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo, ingawa polisi bado hawajathibitisha rasmi. Wabunge kadhaa pia wamekosoa tukio hilo la kurusha kiatu, wakilitaja kama dosari kubwa ya kiusalama.