MR NICE, A MAN OF MANY FIRSTS

Share this story

BONGO Flava kama majira, uvumbuzi na uasisi ni asubuhi, jua la utosi lilipowadia, vipaji kibwena vili-disturb mitaa. Wakati huo sasa, pini “Friday Night” lilipikwa Mawingu Studio kwa Papa Boniluv.

Mgomo fulani hivi, Friday Night ikawa haisikiki redioni. Story ya nyimbo kutupwa kapuni. Legend John Dilinga Matlou “DJ JD”, kwa uthubutu wa kucheza ngoma zilizokataliwa, pini likaanza kubamba. Friday Night ikahit.

Ndivyo Nice Lucas Mkenda, alivyoingia kazini akitumia moniker “Mr Nice”. Anaongea lafudhi ya kizanzibari. Anajua kudance. Akawekeza zaidi kwenye video. Ungemgomea redioni, angesumbua runingani kwa dance performance videos.

Friday Night ilikuwa R&B ya kuchovya. Mr Nice alishitukia mapema R&B isingejaza noti benki. Akajiundia mahadhi yake. Alipoulizwa, Mr Nice unaimba mtindo gani? Alijibu bila kona: “Takeu.”

Akaulizwa tena, Takeu ndiyo nini? Akajibu inawakilisha Tanzania, Kenya na Uganda. Yaani, muziki wa Mr Nice ni made in Tanzania, Kenya and Uganda. Innovator ni Scientist Mr Nice.

Takeu ikaiimbisha Afrika “Kikulacho”. Ikampandisha kuku baiskeli, ikamvalisha bata raizoni katika wimbo “Fagilia”. Mashairi ya “First Lady”, yalikaririwa na watoto kwa wanawake kuliko patriotic song ya “Tazama Ramani”.

Mr Nice ni mwanamuziki wa kwanza Bongo Flava kuwa na seti yake ya dancers. Akatambulisha choreographies za kipekee. Akamleta Wabogojo kwenye kioo, binadamu mithili ya nyoka jinsi anavyonyumbulika na anavyojikunja.

Private jet ni old school story kwa Mr Nice. Mwaka 2004, ratiba imeshona. Anatakiwa Comoros, wakati huohuo anangojewa Washington DC. Promota wa Comoros anaulizwa unaweza kumudu private jet? Akajibu “semeni lingine”. Mr Nice anakwea jet, anatua Maroni, anapiga shoo, anarejea Dar, anapanda passenger aircraft hadi United States of America.

Mr Nice, nywele nyeusi zenye wimbi, TID anaita kokoto. Kwenye gari convertible. Watu wanavunja shingo kumtazama. Kijana mdogo, maarufu sana, fedha ya kutosha. Takeu ilifanya muziki wa Mr Nice ushindane mauzo na tanzanite.

Uvamizi mkubwa uliikumba Takeu. Wanamuziki kibao waliimba Takeu, kuyafuata mamilioni aliyokuwa anayakomba Mr Nice. Hata hivyo, mfalme wa Takeu alibaki mmoja tu; Mr Nice The Millionaire.

Asante sana Bongo Flava Honors Academy kwa kuamua Januari 26, 2024, iwe siku ya kumtunuku Mr Nice heshima yake, vilevile kukumbuka na kutambua mchango wake mkubwa katika ukuaji wa Bongo Flava. Mr Nice ana namba moja nyingi kwenye Bongo Flava. Yes, he’s a man of many firsts.

Tukutane kiotani Alliance Francaise, Upanga, Dar es Salaam.

Nukuu ya Ndimi Luqman MALOTO kupitia ukurasa wa Fb


Share this story

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Previous post DEFENDING CHAMPIONS SENEGAL BEAT CAMEROON 2-1
Next post President William Ruto and his predecessor Uhuru Kenyatta shake hands during the inauguration of DRC President Felix Tshiseked