Alikiba anawataka walio na umri wa zaidi ya miaka 80 kujifunza kutokana na kifo cha Raila na kufurahia maisha
Msanii wa muziki nchini Tanzania Ali Saleh Kiba, almaarufu Alikiba, amewataka wazee hasa walio na umri wa zaidi ya miaka 80 kukumbatia maisha na kupata furaha, wakitafakari kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Akizungumza kutoka Nairobi siku ya Jumamosi, Oktoba 18, 2025, ambako ameratibiwa kutumbuiza Jumapili, Oktoba 19, 2025, Alikiba alisema kuwa kufikisha umri mkubwa ni zawadi na inafaa kuthaminiwa
“Mara mtu anapofikisha miaka 80 na zaidi, lazima uwe na furaha sana kwa sababu uzee ni zawadi,” Ali alisema.
Mkali huyo wa hit song ‘Mapenzi Run Dunia’ alieleza kuwa maisha yanaweza kuwa tete, huku akikumbuka kuwa watu wengi hufa wakiwa wadogo, wakati mwingine wakiwa na umri wa kuanzia miaka thelathini, arobaini au hata ujana na kuacha ndoto zisizotimia.
“Kuna watu wanaofariki wakiwa na umri wa miaka mitatu, minne au hata kumi, bado wangali wadogo,” aliongeza.
Alikiba alitofautisha hili na maisha marefu ya Raila Odinga, akibainisha kuwa kuaga kwake katika umri mkubwa kulibeba somo kwa wale ambao wameishi muda mrefu zaidi.
Alisisitiza kuwa Raila amepata mafanikio makubwa, sio tu nchini Kenya bali kote barani Afrika, ambapo anatambulika kama mtu mashuhuri katika harakati za kupigania uhuru, haki na maendeleo.
“Maumivu ni maradufu mtu anapokufa akiwa mchanga. Baba yetu ametuacha tukiwa tumeishi maisha kamili. Alitufundisha mambo mengi na akafanikiwa mengi kwa sababu Afrika yote inamtambua kama mtu mashuhuri aliyepigania uhuru,” Ali aliongeza.
.