Majaji wapya 15 wa Mahakama ya Rufaa waapishwa
Rais William Ruto leo Jumatano ameongoza hafla ya uapisho wa majaji wapya 15 walioteuliwa kujiunga na Mahakama ya Rufaa.
Hafla ya kuwaapisha majaji hao ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi.
Jaji Mkuu Martha Koome ambaye pia ni Rais wa Mahakama ya Upeo aliwaongoza maafisa wengine wa Idara ya Mahakama katika kuhudhuria hafla hiyo.
Akizungumza wakati wa uapisho huo, Rais Ruto aliwapongeza majaji hao kwa uteuzi wao akisema kwa kukubali kujiunga na mahakama hiyo, wanajiunga na taasisi muhimu ambayo nguvu yake, uhuru na uaminifu ni muhimu kwa uthabiti wa nchi.
Ruto alielezea dhamira ya utawala wake kuboresha utenda kazi wa Idara ya Mahakama akiongeza kuwa kufikia mwezi Machi mwaka huu, majaji wengine watateuliwa kuhudumu katika Mahakama Kuu.
Hata hivyo, alielezea hulka ya idara hiyo kuwa kikwazo kwa utekelezaji wa sera za serikali.