
KQ Yadhibitisha Kifo Cha Abiria Ikiwa Angani
Ndege ya Shirika la Ndege la Kenya Airways iliyokuwa ikitoka New York kwenda Nairobi ilikumbwa na mkasa siku ya Ijumaa baada ya abiria mmoja kuaga dunia angani baada ya kupata dharura ya kiafya.
Kulingana na taarifa kutoka kwa shirika la ndege la Kenya, kisa hicho kilitokea kwenye Ndege ya KQ 003, iliyokuwa imetoka katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy mjini New York kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi.
Licha ya matumizi ya vifaa vya matibabu vilivyokuwa ndani ya ndege abiria huyo alitangazwa kufariki saa 9:10 asubuhi, kabla ya ndege hiyo kutua.
Ndege hiyo ilitua JKIA saa 10:27 asubuhi, ambapo ilikutana na wahudumu wa afya, usalama wa uwanja wa ndege na Mamlaka nyingine za serikali.
