
Kalonzo Afichua Mpango Wa Ruto na Raila Kuvuruga Uchaguzi Wa 2027
Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amejitokeza na kufichua mipango ya Rais William Ruto na mwandani wake Raila Odinga ya kuvuruga uchaguzi ujao wa 2027.
Kupitia taarifa, Kalonzo alibainisha kuwa uteuzi wa IEBC ulikuwa ‘upanuzi wa kisiasa wa Ikulu—ukiwa na wafuasi watiifu wa Ruto na washauri wake.’
“Tulichohofia sasa kimetimia. Rais William Ruto amechagua mrengo wa IEBC-iliyoundwa kutimiza azma yake ya kuchaguliwa tena 2027. Hii si tume ya wananchi. Ni mradi uliobuniwa kuvuruga uchaguzi ujao mchana kweupe, kwa idhini ya mshirika wake mpya, Mhe. Raila Odinga.
“Kanuni za kikatiba za mashauriano, ushiriki wa umma, na kutoegemea upande wowote kisiasa zilitupiliwa mbali kabisa. Matokeo? Tume iliyoathiriwa isiyo na uadilifu, uhalali na uaminifu wa umma”. Yasoma taarifa hiyo
Kalonzo sasa ametaka kuchapishwa kwa ripoti ya kuondoka na rekodi zote za Hansard na jopo la uteuzi lililotwikwa jukumu la kuwaajiri mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na wanachama wa tume hiyo.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari mnamo Jumanne, Mei 13, Kalonzo alisema rekodi hizo zitasaidia Wakenya kuchunguza vigezo vilivyotumiwa na jopo la uteuzi kupendekeza uteuzi wa mwenyekiti wa IEBC na wanachama wa baraza la uchaguzi.
“Tunataka kuchapishwa mara moja na kamili kwa ripoti ya kuondoka kwa Jopo la Uteuzi na rekodi zote za Hansard ambazo umma unaweza kuchunguza kwa vigezo vilivyotumiwa na jopo la uteuzi kupendekeza wateule 6 wa tume,” ilisoma taarifa hiyo kwa sehemu.


