De Rossi apigwa kalamu na AS Roma

Share this story

AS Roma imempiga kalamu kocha wao Daniele De Rossi baada ya matokeo mabaya kwa mechi nne za mwanzo wa msimu wa 2024/25 katika Ligi ya Serie A.

Roma imetoka sare mechi tatu na kupoteza moja. Imetoka sare dhidi ya Cagliari, Juventus na Genoa. Ilichapwa na Empoli.

De Rossi alijiunga na Roma mwezi Januari mwaka huu kuchukua nafasi ya Jose Mourinho aliyepigwa kalamu pia. Kwa sasa Roma wako nambari ya 16 kwenye jedwali na alama tatu.

Baada ya De Rossi kujiunga na Roma timu hiyo ilitoka katika nambari ya tisa na kukamilisha msimu wa 2023/24 kwenye nafasi ya sita.

Pia alisaidia timu hiyo kufika nusu fainali ya Ligi ya Europa ambapo waliondolewa na Bayer Leverkusen. Roma walifuzu Ligi ya Europa baada ya kuwa ya sita.

Roma imetoa sababu ya kumfuta De Rossi.

“Uamuzi wa klabu unachukuliwa kwa maslahi ya timu, kuweza kuanza mara moja njia inayotakiwa wakati ambapo msimu bado upo mwanzoni,” ilisema Roma kupitia ujumbe.

“Kwa Daniele, ambaye daima atakuwa nyumbani katika klabu ya Giallorossi, shukrani za dhati kwa kazi iliyofanywa katika miezi hii kwa ari na kujitolea.”

Uamuzi huu wa kumtimua De Rossi umetokea licha ya kutia saini mkataba mpya hadi mwaka wa 2027 hivi majuzi.

Roma inatarajia kusajili ushindi wa kwanza wa msimu Jumapili ijayo dhidi ya Udinese nyumbani.

Akiwa mchezaji, De Rossi ambaye alicheza safu ya kati alikuwepo Roma kwa miaka 18 ambapo alicheza mechi 600.

Klabu hiyo ya Serie A sasa itakuwa inamtafuta kocha wao wa nane katika kipindi cha miaka 11 huku wakiendelea kutatizika kudumisha uthabiti na maisha marefu dimbani.


Share this story

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Previous post Tanzania’s Yanga to play Gor Mahia in Siaya
Next post Junior Harambee Starlets depart for Spain ahead of World Cup